Watafiti katika Chuo Kikuu cha Cambridge waliweza kuwafundisha kondoo kutambua nyuso za watu mashuhuri wakiwemo waigizaji Jake Gyllenhaal na Emma Watson, rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mtangazaji wa BBC Fiona Bruce.
Baada ya mafunzo, kondoo walionekana kuchagua picha za nyuso walizozifahamu awali mara nyingi.
Hii inadhihirisha kwamba kondoo wana uwezo wa kutambua na kutofautisha nyuso za watu sawa na wanyama wa familia ya binadamu, tumbili na sokwe.
Utafiti wa awali ulikuwa umedhihirisha kwamba kondoo huweza kutambua na kutofautisha nyuso za kondoo wengine na pia watu wanaowatunza.
"Tulichofanya ni kuuliza iwapo kondoo wanaweza kumtambua mtu kutoka kwenye picha," mtafiti mkuu Prof Jenny Morton amesema.
"Tuliangazia kuhusu iwapo ni kweli au la wanyama wanaweza kufasiri kitu ambacho kina upana na urefu (2D) pekee kwamba ni mtu huyo."
Kondoo jike wanane walifunzwa kutofautisha nyuso za watu wanne mashuhuri kutoka kwa mkusanyiko wenye picha za watu wasiowafahamu kwa kutumia chakula kama zawadi.
Kondoo hao walionyeshwa picha tofauti kwenye vioo vya kompyuta mbili; walifanya uteuzi wao kwa kuzuia miali ya infrared kwa kutumia pua na hapo zawadi yao ya chakula ikatolewa.
Baada ya kubainisha uwezo wa mifugo hao kuwatambua watu hao mashuhuri, watafiti hao waliwawekea mtihani mwingine sasa.
Walitaka kujua iwapo wanyama hao wangewatambua watu hao kutoka kwenye upande tofauti.
Kwa mara nyingine, waliweza.
Sign up here with your email