Sign up here with your email
Utafiti: Manchester City wana nafasi nzuri ya kushinda ligi England
Ligi ya Premia msimu huu imechezwa mechi saba pekee, lakini tayari kuna klabu kadha ambazo zimeanza kujitokeza kuonyesha matumaini ya kufanikiwa kushinda ligi msimu huu.
Kampuni ya data ya Gracenote Sports, ambayo huangazia zaidi ubashiri wa matokeo ya mechi, imebadilisha ubashiri wake kuhusu nani atashinda ligi msimu huu kutoka kwa Chelsea hadi kwa Manchester City.
Aidha, wanabashiri kwamba Crystal Palace wataendelea kushika mkia na kushushwa daraja mwisho wa msimu.
Gracenote hutumia mfumo wake wa kuorodhesha klabu wa Euro Club Index kuorodhesha klabu mbalimbali, na kisha hutumia kompyuta za kubashiri matokeo ya mechi msimu mzima mara milioni moja kubashiri jinsi jedwali litakuwa mwisho wa msimu.
City watawapiku United
Chelsea walikuwa wanapigiwa upatu mwanzoni mwa msimu nao City walitarajiwa kumaliza wa pili na United nambari tano.
Lakini klabu hizo mbili za Manchester zimeanza kwa kishindo msimu huu na matokeo yao karibu yanakaribiana.
Ni tofauti ya mabao pekee ambayo inawawezesha City wakiwa na Pep Guardiola kuwa kileleni.
City wamepewa nafasi ya 47% kushinda ligi, United nafasi ya 24% na Chelsea 13%.
Spurs wanatarajiwa kuwa nafasi ya nne nao Arsenal nafasi ya tano na Liverpool nafasi ya sita